Historia

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi- Nachingwea (MANAWASA) iliundwa rasmi kupitia tangazo  la serikali namba 105 la tarehe 10/05/2013. Kabla ya kuundwa kwa MANAWASA kulikuwa na Mamlaka za maji mbili zilizoitwa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Masaji Mjini (MAUWASA) pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Nachingwea Mjini (NAUWASA) ambazo zilikuwa zinatoa huduma katika Mji wa Masasi (Mkoa wa Mtwara) na Mji wa Nachingwea (Mkoa wa Lindi). MANAWASA ni miongoni mwa Miradi Saba ya Kitaifa ambayo inatoa huduma ya kusambaza maji na usafi wa mazingira katika Miji ya Masasi , Nachingwea  pamoja na vijiji vya wilaya ya Ruangwa ambavyo vimepitiwa na bomba kuu la usambazaji maji.  Hata hivyo kupitia zoezi la kuunganisha Mamlaka za maji kama ilivyoelezwa kwenye sheria ya Maji Na.5 ya Mwaka 2019, MANAWASA imeongezewa Wilaya ya Nanyumbu (Mangaka) kwa mujibu Tangazo la Serikali lenye GN Na.826 ya mwaka 2019.  Mamlaka ina kanda mbili, Wilaya ya Masasi na Kanda ya Nachingwea yenye makao makuu yake Wilaya ya Masasi, na kanda ya tatu ya Kijijini pia itaanzishwa.

MANAWASA ipo kundi C. Kwa tafsiri, Mamlaka ya maji ya Kundi C ni Mamlaka ambayo inatoa huduma ya maji ya chini ya 65% na inakidhi gharama zote za uendeshaji na matengenezo isipokuwa sehemu ya gharama za umeme wa mitambo kama ilivyobainishwa katika Mkataba wa Maelewano uliotiwa saini kati ya Wizara ya Maji na Mamlaka. Kuwa Mamlaka ya kundi C na mradi wa Kitaifa kama mradi mwingine wa kitaifa, serikali ya Tanzania ina wajibu wa kusaidia Mamlaka hizi katika kufadhili miradi yake ya uwekezaji kama vile upanuzi wa mabomba ili kuongeza wigo wa huduma. Mamlaka  ina wajibu wa kusambaza majisafi na salama na kukusanya maji taka  katika Miji ya Masasi, Nachingwea,Mangaka pamoja na vijiji vilivyopitiwa na bomba kuu la Maji kutokea kwenye vyanzo vya Maji Mbwinji sambamba na vijiji Nane (8) vilivyopo kwenye Wilaya ya Ruangwa. Aidha kupitia Tangazo la Serikali lenye GN Na.826 ya mwaka 2019 MANAWASA imekabidhiwa jukumu la kuilea Mamlaka ya Maji ya Ruangwa.